Jumanne 15 Septemba 2026 - 13:21
Operesheni ya “Sharurah” lilikuwa ni shambulizi la kushtukiza la kimkakati; Kukata njia za ugavi wa adui ni ufunguo wa mabadiliko yajayo

Hawzah/ Meja Jenerali Khalid Gharab amesema kuwa kumalizika kwa vita vya pwani ya magharibi ndani ya siku saba, kudhibiti wilaya sita na kuvunja mikusanyiko ya majeshi ya adui wa Saudi Arabia, kumeonesha mabadiliko makubwa katika utendaji wa kijeshi.

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Meja Jenerali Khalid Gharab, mtaalamu wa kijeshi wa Yemen, katika mahojiano na kipindi cha “Nawafidh” kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Al-Masirah, amesisitiza kwamba; operesheni ya Yemen iliyolenga eneo la “Sharurah” ilimshtukiza adui, na kwamba lengo lake lilikuwa kukata njia za usafirishaji wa vifaa na silaha.

Amesema kuwa; Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen, katika kipindi cha miezi kadhaa na kupitia mapigano yaliyotangulia, vilijikusanyia uzoefu mkubwa wa kivita, jambo lililoviwezesha kutekeleza majukumu yao katika mazingira na maeneo yenye miinuko na hali tofauti za kijiografia.

Meja Jenerali Gharab ameeleza kwamba hali ya maeneo na miinuko inaweza kuwa kikwazo katika baadhi ya mapigano, lakini mafunzo na uzoefu uliopatikana uliviwezesha vikosi kufanya operesheni katika maeneo ya milimani, tambarare na mabonde. Urahisi wa maeneo na hali ya kijiografia huwapa wapiganaji uwezo na ubora zaidi katika utendaji wao wa uwanjani.

Amebainisha kwamba; kumalizika vita vya pwani ya magharibi ndani ya siku saba, kudhibiti wilaya sita zenye eneo linalokadiriwa kuwa karibu kilomita za mraba 5,400, pamoja na kuvunjwa vikosi 38 miongoni mwa mikusanyiko ya adui wa Saudi Arabia, ni dalili ya mabadiliko makubwa katika utendaji wa kijeshi na kunalazimisha pande zote kufanya mapitio ya hesabu zao kuhusu aina ya operesheni zinazokuja.

Gharab amesema kuwa; maendeleo ya hivi karibuni katika pwani ya magharibi yameonesha kwamba kulenga maghala ya silaha, misafara ya kijeshi na maeneo yaliyokuwa yakitumiwa na vikosi vya adui kumeanza. Ameitaja operesheni hiyo kuwa sehemu ya muktadha huo na kuielezea kama ujumbe muhimu wa kijeshi, kwa sababu eneo hilo lina uhusiano na vituo vya kukusanyia wanajeshi, vituo vya ugavi na maeneo ya kukusanyika kwa vikosi. Aidha, kulenga maeneo ya ugavi na silaha huathiri moja kwa moja uwezo wa kuendelea operesheni za kijeshi.

Amesisitiza kwamba; kuzuiwa vifaa vya ugavi, iwe ni vya kijeshi au vya chakula, husababisha kudhoofika uwezo wa kikosi chochote kuendelea kuwepo katika mazingira ya mapigano. Operesheni zilizotangazwa hadharani na vyombo vya habari, zikiwemo kulengwa mikusanyiko na misafara ya kijeshi, zinaonesha kwamba operesheni hizo zimeingia katika hatua pana zaidi ya kutoa mashambulizi yenye madhara makubwa.

Mtaalamu huyo wa kijeshi amebainisha kwamba; mfululizo wa operesheni, kuanzia mashambulizi ya makombora ya balestiki hadi matumizi ya ndege zisizo na rubani, pamoja na kulengwa maeneo muhimu, maghala ya silaha na maeneo ya kukusanyia wanajeshi, unafanyika katika mfumo wa operesheni za kuzuia mashambulizi mapema, kwa lengo la kuvuruga maandalizi ya kijeshi na kuyazuia mashambulizi kabla hayajatekelezwa. Amesema kuwa; hali ya mapigano yanayokuja, hususan katika maeneo ya mashariki, itavipa Vikosi vya Wanajeshi vya Yemen ubora zaidi wa uwanjani, kutokana na hali ya maeneo na miinuko pamoja na uzoefu ambao vikosi hivyo vimeupata kutokana na mapigano yaliyotangulia.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha